Save the Children: Msichana wa chini ya miaka 15
huozwa 'kila sekunde saba'
- 11 Oktoba 2016
India ni moja ya nchi ambazo zinaongoza kwa visa vya ndoa za watoto,
ripoti hiyo inasema
Ripoti mpya ya shirika la Save the
Children inasema msichana wa chini ya miaka 15 huozwa kila baada ya sekunde
saba duniani.
Ripoti hiyo inasema watoto wa hadi
chini ya miaka 10 wanashurutishwa kuolewa na wanaume wazee katika nchi kama
vile Afghanistan, Yemen, India na Somalia.
Save the Children wanasema ndoa za
mapema zinaweza kuchangia msururu wa matatizo ambayo huathiri maisha yote ya
msichana.
Mizozo, umaskini na migogoro ya
kibinadamu vinatazamwa kama sababu kuu zinazowaweka wasichana hatarini ya
kuozwa wakiwa bado wana umri mdogo.
"Ndoa za mapema huanzisha
msururu wa matatizo ambayo humnyima msichana haki za kimsingi za kujifunza,
kujikuza na kujivunia maisha yake kama mtoto," amesema afisa mkuu mtendaji
wa Save the Children International Helle Thorning-Schmidt.
"Wasichana wanaoolewa wakiwa
wadogo mara nyingi huwa hawawezi kuendelea na masomo, mara nyingi hudhulumiwa
na waume zao, kupigwa na hata kunyanyaswa kingono. Hupachikwa mimba na pia huwa
hatarini ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa, ukiwemo Ukimwi."
Ripoti hiyo iliyopewa jina Every
Last Girl, imeorodhesha nchi ambazo ni ngumu zaidi kwa wasichana baada ya
kuzingatia elimu, ndoa za watoto, mimba za mapema, vifo vya wanawake
wakijifungua na idadi ya wanawake bungeni.
Chad, Niger, Jamhuri ya Afrika ya
Kati, Mali na Somalia zinashika mkia kwenye orodha hiyo.
Image copyright Getty Images Image
caption Ripoti hiyo inasema wasichana kwenye kambi za wakimbizi wamo hatarini
ya kuozwa wakiwa wadogo
Shirika la Umoja wa Mataifa
linalowashughulikia watoto, Unicef, linakadiria kwamba idadi ya watoto
watakaoozwa wakiwa wadogo itaongezeka kutoka 700 milioni kwa sasa hadi 950
milioni kufikia 2030.
Ripoti hiyo ya Save the Children
imetolewa siku ya maadhimisho ya Siku ya Msichana Duniani.