Thursday 19 December 2019

JINSI YA KUPOTEZA UPEKEE WA MWENZA WAKO

‘’Ninatamani mke/mume wangu angekuwa kama fulani, ninatamani ndoa yetu ingekuwa kama kina fulani , kama tungekuwa na kitu x kama kina fulani tungekuwa … ni baadhi ya maneno ya wanandoa ambao hawajui kuwa maneno kama hayo huwa ni sumu kwenye mahusiano yao.

Katika mahusiano ya ndoa, kama wanandoa wakishaanza kulinganishana na wengine, yaani kila mmoja anatamani mwenza wake angekuwa kama fulani hapo ndiyo mahali unapoanza kupoteza upekee wa mwenza wako.

Njia rahisi ya kupoteza upekee wa mwenza wako ni kumlinganisha na mwingine. Natamani ungekuwa kama fulani, ni maneno ambayo yanapoteza nguvu sana na kufanya wanandoa kuwa dhaifu. Kamwe usimlinganishe mwenza wako na mtu mwingine.

KAVA IJUE NJAA YA WANANDOA

Tambua kuwa kila mtu ana upekee wake, na ukianza kulinganisha mwenza wako na mtu mwingine ni kumfedhehesha kama siyo kumkosea heshima. Unapomlinganisha mwenza na mtu mwingine ni rahisi kumpotezea nguvu ya kujiamini.

Na kama unavyojua binadamu ni viumbe wa hisia, unapomlinganisha anajihisi kutothaminiwa na hitaji la kila mwanadamu ni kuhisi anathaminiwa.

Ni rahisi kupoteza ladha ya mahusiano yenu pale unapoanza kumfananisha mwenza wako na mtu mwingine. Kama vile chakula kilichokosa chumvi kinakuwa hakina ladha ndivyo ilivyo kwa mahusiano yetu pale tunapokuwa tunataka wenza wetu wawe kama kina fulani tunakuwa tunapoteza tena ile ladha au upekee wao juu yetu.

Huwezi kumpata mtu aliyekamilika kwenye kila eneo la maisha yako, hata wale ambao unawatamani wawe kama mwenza wako nao wana mapungufu mengi tu kushinda hata ya huyo mwenza wako.

Inabidi ifikie mahali urudi kwenye lengo lako kuu la ndoa au mahusiano yenu, kuna kitu ambacho kilikuvuta kwa mara ya kwanza mpaka ukawa na huyo ambaye unaye leo hii hivyo basi siku zote angalia hilo.

Jiulize ilikuwaje au nini kilichokufanya uwe na mwenza uliye naye sasa? Ukiwa ni mtu wa kujihoji utakua na maana kwenye maisha yako ya ndoa lakini mtu ambaye hajioji hana sababu ni mtu ambaye tayari amepoteza maana ya maisha ya ndoa. Lazima uwe na sababu kwenye kila kitu, kwanini unafanya hicho unachofanya sasa unapokuwa na sababu basi unakuwa na maana lakini ukikosa sababu unapoteza maana.

Hatua ya kuchukua leo; usimlinganishe mwenza wako na mtu mwingine yeyote yule. Kumbuka mwenza wako ni wa pekee sana hawezi kuwa kama wengine na unapomlinganisha jua unauwa upekee wake.

Siku zote angalia sababu iliyokufanya uwe na huyo ambaye unaye leo. Usitamani ya watu bali mtengeneze mwenza wako awe vile unavyotaka awe na kwa upendo na umoja mtaliweza hilo.

Hivyo basi, wakati mwingine tunatakiwa kuchukuliana kwenye maisha ya ndoa, tuwavumilie wenzetu kadiri ya madhaifu yao, tuangalie mazuri yao na kuyatumia vema , lakini tukiweka fokasi yetu kwenye mabaya tutazidi kuona mabaya yao kila siku na mwisho wa siku mtachokana haraka.

Maisha ya ndoa ni maisha mafupi sana hivyo ni vema mkapendana kwa muda kwani wengi mnakutana tayari mmeshakuwa watu wazima na mkiishi mtaishi kwa muda tu kumalizia safari ya maisha yenu hapa duniani.

Saturday 23 November 2019

HESHIMA NDIYO UTI WA MGONGO WA NDOA

Hakuna kitu kimoja peke yake kinaweza kuifanya ndoa yako kuwa bora. Bali mkusanyiko wa mambo madogo madogo ya kila siku ndiyo yanaweza kujenga au kubomoa ndoa.

Hakuna mtu ambaye ameamka akajikuta na tabia ambayo anayo sasa katika ndoa yake. Tabia zote tulizonazo katika mahusiano yetu tumezitengeneza sisi wenyewe iwe ni tabia nzuri au mbaya bali sisi ndiyo wazazi wa tabia ambazo tunazo sasa.
Katika shabaha ya makala yetu ya leo tunakwenda kujifunza utii wa mgongo wa ndoa.
Uti wa mgongo wa ndoa yako ni heshima. Unapoheshimika heshimika.

Mwenzako anapowahi kurudi nyumbani hapo amekuheshimu. Heshima ni kitu cha bure wala hakihitaji mtaji.

Unapomheshimu mwenzako kwa yale mambo madogo naye anakuheshimu pia.
Leo ni vigelele kesho isiwe kelele.

Thamini kile anachofanya mwenzako, kwa kufanya hivyo unakuwa unamweshimu mwenzako.
Unapompenda mwenzako unakuwa unamweshimu. Hivyo kumpatia mwenzako upendo ni kumpa dozi ya heshima.
Ukiheshimiwa jiheshimu. Hapa unatakiwa kujiheshimu hata uvaaji wako, tembea yako ioneshe kama vile vile wewe ni mke au mume wa mtu.

Huwa tunajidharirisha sisi wenyewe kwa namna nyingi, unapokuwa mlevi kwa mfano, ukalewa mpaka kujikojolea hapo unapokuwa umemdharirisha mwenzako na kumvunjia heshima.
Unapomshirikisha mwenzako wa ndoa katika mipango yako hapo unakuwa una mweshimu na yeye atakuheshimu pia na kwa kukushirikisha mipango yake.

Unapomuaga mwenzako au kumjulisha kuwa leo utachelewa kufika nyumbani kwa kitendo Kama hiko hapo utakuwa unamweshimu mwenzako wa ndoa.
Nyumba zinaungua usiku mchana zinakuwa vizuri ni methali ya kihaya, hapo ina maana kwamba hata kama mnatofauti zenu mzimalize ndani na mkiwa nje muwe vizuri.
Hatua ya kuchukua leo; mweshimu sana mwenzako wa ndoa. Mpe dozi ya upendo na msikilizane kwa upendo na kuheshimiana kila siku.
Kwahiyo, hakuna kitu kidogo katika ndoa. Thamani yoyote unayoitoa kwa mwenzako inakuwa ni heshima na heshima inakuwa ni uti wa mgongo wa ndoa yako.