Sunday 5 June 2016

VIKWAZO VITANO { 5} VINAVYOHARIBU MAHUSIANO YETU NA NDOA ZETU NA JINSI YA KUVIEPUKA



Tunapenda kujifunza kila siku ili tuweze kuijua kweli nayo kweli itatuweka huru. Kama hujui ukweli utapata shida kwani jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Katika maisha yetu ya kila siku tunakumbana na vikwazo mbalimbali. Sasa leo naomba tujifunze vikwazo ambavyo vinaweza kuharibu ndoa yako. Siyo tu maisha ya ndoa hata uchumba na maisha yoyote yenye mahusiano.
Binadamu ni mtu mwenye asili ya mahusiano hapa duniani. Kama wewe ni binadamu basi huwezi kukwepa mahusiano mfano mahusiano na wazazi wako, familia yako, ndugu, jamaa na marafiki.


Vifuatavyo ni vikwazo katika maisha ya ndoa, mahusiano mengine na jinsi ya kuviepuka.

1. Uchafu;
Kila mtu anapenda kuona sehemu anayokaa ni safi au mazingira aliyopo ni safi, vyombo tunavyotumia wakati wa kula, sehemu unayolala, nguo unazovaa, usafi wa mwili nakadhalika. Mtu ambaye ni mchafu huwa ni kikwazo kwa watu wengine anaoishi nao iwe ni katika mahusiano ya kifamilia au ndoa.
Kwa wale watu ambao wako katika maisha ya ndoa kitu kinachoitwa usafi ni jambo la msingi sana na la kuzingatia na siyo kitu siku cha moja bali ni kitu cha siku zote. Wanandoa wote wawili wanapaswa kuzingatia usafi katika maisha yao. Swala la usafi ni katika maeneo yote kuanzia mwili, nguo, sehemu unayolala nakadhalika. Wapo watu wengi wanaharibu ndoa zao kwa sababu tu ya uchafu wewe kama ni mke au mme unaweza kumkwaza mwenza wako kama wewe ni mchafu yaani mtu ambaye hupendi usafi.
Hatua ya kuchukua;
Kama ulikuwa ni mchafu anza sasa kuwa msafi ili ulinde mahusiano yako. Kuwa msafi wa kila kitu usidharau hata kitu kimoja. Kama ulikuwa ni mtu wa kuvaa nguo bila ya kutofautisha nguo hizi ni za kutokea, shamba, kushindia, kulalia anza leo kuvaa kulingana na wakati wa shughuli husika.
Kama wewe ni mchafu wa kinywa basi safisha kinywa chako kila siku ili usiwe kero kwa mwenza wako na hata watu wengine. Uchafu ni hasara katika mahusiano hivyo kuwa msafi wa mwili, akili nk. na usafi ni faida katika mahusiano.



2.Uvivu;
Ashakumu si matusi ndugu msomaji, uvivu ni kama mavi. ‘’mvivu hufanana na jiwe litiwalo mavi, kila mtu atamfyonya katika aibu yake. Mvivu hufanana na uchafu wa jaani, kila augusaye atakung’uta mkono’’ Uvivu ni mbaya sana kama umeweza kufananishwa na kinyesi basi ujue uvivu ni mbaya. Uvivu ni mbaya sana katika maisha ya ndoa na hata maisha mengine kwani uvivu unaleta athari mbaya sana katika maisha yetu ya kila siku. Kama katika maisha ya ndoa wewe ni mvivu basi ni dhahiri kabisa utaweza kuharibu mahusiano ambayo unayo leo hii.
Mtu mmoja aliwahi kusema unaweza kukwepa wajibu wako lakini huwezi kukwepa matokeo ya majukumu au wajibu wako.
Hatua ya kuchukua; anza kufanya mambo yako bila kuahirisha, kuwa na ratiba na ukiweka ahadi ya kufanya jambo hakikisha unalitimiza. Dawa ya uvivu ni kuchukua hatua kwa vitendo bila kusubiria. Kila kitu kinawezekana kama ulikuwa ni mvivu wa kuamka mapema asubuhi basi anza zoezi hilo kwa siku 30 na uvivu utaisha wenyewe. Na hapa unahitaji uwe dikteta wa mwili wako hata kama mwili wako haujisikii kufanya jambo kuwa dikteta na wala usiupe demokrasia mwili wako katika kufanya jambo.

3. Ugomvi;
Ugomvi siyo kitu kizuri na siyo alama nzuri katika maisha ya ndoa hata maisha mengine pia, mfano baba na mama kupigana. Ugomvi unaleta athari katika mahusiano mfano kama mama au baba katika familia ni wagomvi wanaleta athari kubwa hata katika malezi ya watoto kwani watoto wanakuwa hawajifunzi somo zuri kupitia wazazi wao.
Ugomvi unaweza kuwa kikwazo kwa wanandoa na kupelekea kuharibu mahusiano yao.
Hatua ya kuchukua;
Ugomvi siyo picha nzuri katika mahusiano. Kama ulikuwa na tabia hii ni vema ukaiacha na kuanza kuishi maisha ambayo yanampendeza mwenzako, familia yako, hata jamii inayokuzunguka.

4. Ulevi ;
Yule ambaye ni mlevi kati ya wanandoa anakuwa kikwazo kwa mwenza wake. Ulevi wa kupindukia ni athari katika mahusiano ya ndoa na hata watu wengine. Mwenzako anaweza kukerwa na tabia ya ulevi na kupelekea kuharibu mahusiano yenu.
Ulevi unapelekea watu kusahau majukumu yao katika ndoa zao, familia nk. Ulevi ni utumwa ambao unakufanya kuishi maisha ya ajabu sana.
Hatua ya kuchukua;
Achana na ulevi ili kuokoa mahusiano yako ya ndoa. Anza kusema hapana kubwa kwa ulevi kwani unaharibu mahusiano yako ya kifamilia na hata jamii kiujumla.


5. Ukali;
Ukali ni fedheha mbele ya mwenzako. Kuna watu wanaonyesha ukali kwa mke wake au mme wake mbele ya watu. Ukali unageuka kuwa fedheha endapo unamsema mwenzako mbele ya watu tena kwa sauti kubwa ambayo kila mtu anasikia. Hiki ni kikwazo kwa wanandoa. Pia ukiwa mkali sana ni athari hasi tena kwa malezi ya watoto, watoto wanaweza wakakukimbia nyumbani na kuleta chuki miongoni mwa mzazi na mtoto. Baba kumsema mama kwa ukali mbele ya watoto nayo ni athari mbaya kwani unajenga picha mbaya kwa watoto wanaokuwa na kuhitaji kupata mwongozo kutoka kwa wazazi wao.

Hatua ya kuchukua;
Ukiwa katika hisia kama vile kuwa na hasira usifanye maamuzi yoyote tulia kwanza mpaka hasira zako ziishe. Kama ulikuwa na tabia ya ukali na kumsema mwenzako mbele ya watu siyo tabia nzuri kwani ni fedheha kubwa na hivyo acha kabisa tabia hiyo katika hali ya kawaida ambayo inampendeza mwenzako na familia yako kiujumla.
Mwisho; katika mahusiano kila mtu ni mteja kwa mwenzako angalia vile vitu ambavyo hupendi kufanyiwa wewe basi usimfanyie mwenzako kwani inakuwa ni kero na kikwazo kwa mwenzako. Kama tulivyoona hivyo vikwazo hapo juu ni tabia ambazo mtu hajazaliwa nazo hivyo ana uwezo wa kuziacha na kuendelea na maisha yanayostahili kuishi.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe  deokessy.dk@gmail.com  au  unaweza  kutembelea  tovuti  yake   www.actualizeyourdream.blogspot.com

No comments:

Post a Comment