‘’Ninatamani
mke/mume wangu angekuwa kama fulani, ninatamani ndoa yetu ingekuwa kama
kina fulani , kama tungekuwa na kitu x kama kina fulani tungekuwa … ni
baadhi ya maneno ya wanandoa ambao hawajui kuwa maneno kama hayo huwa ni
sumu kwenye mahusiano yao.
Katika mahusiano ya ndoa, kama
wanandoa wakishaanza kulinganishana na wengine, yaani kila mmoja
anatamani mwenza wake angekuwa kama fulani hapo ndiyo mahali unapoanza
kupoteza upekee wa mwenza wako.
Njia rahisi ya kupoteza upekee wa
mwenza wako ni kumlinganisha na mwingine. Natamani ungekuwa kama
fulani, ni maneno ambayo yanapoteza nguvu sana na kufanya wanandoa kuwa
dhaifu. Kamwe usimlinganishe mwenza wako na mtu mwingine.
KAVA IJUE NJAA YA WANANDOA
Tambua
kuwa kila mtu ana upekee wake, na ukianza kulinganisha mwenza wako na
mtu mwingine ni kumfedhehesha kama siyo kumkosea heshima.
Unapomlinganisha mwenza na mtu mwingine ni rahisi kumpotezea nguvu ya
kujiamini.
Na kama unavyojua binadamu ni viumbe wa hisia,
unapomlinganisha anajihisi kutothaminiwa na hitaji la kila mwanadamu ni
kuhisi anathaminiwa.
Ni rahisi kupoteza ladha ya mahusiano yenu
pale unapoanza kumfananisha mwenza wako na mtu mwingine. Kama vile
chakula kilichokosa chumvi kinakuwa hakina ladha ndivyo ilivyo kwa
mahusiano yetu pale tunapokuwa tunataka wenza wetu wawe kama kina fulani
tunakuwa tunapoteza tena ile ladha au upekee wao juu yetu.
Huwezi
kumpata mtu aliyekamilika kwenye kila eneo la maisha yako, hata wale
ambao unawatamani wawe kama mwenza wako nao wana mapungufu mengi tu
kushinda hata ya huyo mwenza wako.
Inabidi ifikie mahali urudi
kwenye lengo lako kuu la ndoa au mahusiano yenu, kuna kitu ambacho
kilikuvuta kwa mara ya kwanza mpaka ukawa na huyo ambaye unaye leo hii
hivyo basi siku zote angalia hilo.
Jiulize ilikuwaje au nini
kilichokufanya uwe na mwenza uliye naye sasa? Ukiwa ni mtu wa kujihoji
utakua na maana kwenye maisha yako ya ndoa lakini mtu ambaye hajioji
hana sababu ni mtu ambaye tayari amepoteza maana ya maisha ya ndoa.
Lazima uwe na sababu kwenye kila kitu, kwanini unafanya hicho
unachofanya sasa unapokuwa na sababu basi unakuwa na maana lakini
ukikosa sababu unapoteza maana.
Hatua ya kuchukua leo;
usimlinganishe mwenza wako na mtu mwingine yeyote yule. Kumbuka mwenza
wako ni wa pekee sana hawezi kuwa kama wengine na unapomlinganisha jua
unauwa upekee wake.
Siku zote angalia sababu iliyokufanya uwe na
huyo ambaye unaye leo. Usitamani ya watu bali mtengeneze mwenza wako awe
vile unavyotaka awe na kwa upendo na umoja mtaliweza hilo.
Hivyo
basi, wakati mwingine tunatakiwa kuchukuliana kwenye maisha ya ndoa,
tuwavumilie wenzetu kadiri ya madhaifu yao, tuangalie mazuri yao na
kuyatumia vema , lakini tukiweka fokasi yetu kwenye mabaya tutazidi
kuona mabaya yao kila siku na mwisho wa siku mtachokana haraka.
Maisha
ya ndoa ni maisha mafupi sana hivyo ni vema mkapendana kwa muda kwani
wengi mnakutana tayari mmeshakuwa watu wazima na mkiishi mtaishi kwa
muda tu kumalizia safari ya maisha yenu hapa duniani.
BLOGU HII NI MAALUMU KWA WALE AMBAO WAPO KATIKA MAHUSIANO YA URAFIKI , UCHUMBA , NDOA . JIFUNZE MBINU ZA KUDUMISHA MAHUSIANO YAKO YA URAFIKI , UCHUMBA NA NDOA. PATA MAJIBU KWA NDOA YAKO. " UPENDO HAUNA MWISHO, HAYA NAWAAMURU NINYI KUPENDANA. ENYI WAUME , WAPENDENI WAKE ZENU." (WAKORINTHO 13:8 , YOHANA 15:17 , WAEFESO 5 :25).