Ndoa za utotoni janga Tanzania
- 29 Oktoba 2014
Image caption Watoto walioathirika
na ndoa na mimba za utotoni Tanzania
Tanzania ni moja ya nchi zinaoongoza
kwa mimba na ndoa za utotoni, kwa mujibu wa ripoti inayotarajiwa kuzinduliwa
hii leo jijini Dar es Salaam na Shirika la Haki za Binadamu duniani.
Hata hivyo nchi hiyo imepiga
marufuku ndoa hizo, ambapo mtoto wa kike anaruhusiwa kuolewa anapofikisha umri
wa miaka kumi na nane.
Mkoa wa Shinyanga ulio kaskazini
magharibi mwa Tanzania ndio unaotajwa kuongoza kwa mimba na ndoa za utotoni,
ikilinganishwa na mikoa mingine nchini humo.
Takwimu kutoka mashirika mbalimbali
ikiwemo UNICEF zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za
utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii
imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo
ya mtoto wa kike katika eneo hilo.
Ili kumwokoa mtoto wa kike kutokana
na janga hili, kumekuwa na jitihada mbalimbali kutoka mashirika yasiyo ya
kiserikali za kuwaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi
hilo.
Shirika lisilo la kiserikali la
Agape limeweza kuwaokoa wanafunzi wa kike wapatao mia mbili, wakiwa wamepitia
ndoa za utotoni. Wengine tayari wamezalishwa wakiwa na umri chini ya miaka 13.
Hivi sasa wanaanza maisha mapya ya kusoma.
Mmoja wa watoto waliokolewa akiwa
amejitambulisha kwa jina la Pili Omar, ana miaka 14 na ni mama wa mtoto mmoja.
na amekubali kueleza kilichomsibu."Niliolewa kwa sababu wazazi wangu
waliniambia sitaendelea kuwa mzigo kwao, hivyo niolewe ili nianzishe mji
wangu."anasema Pili.
Wazazi na walezi wa watoto hawa
wanalaumiwa kwa kuwalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa za utotoni. Licha
ya kukithiri kwa ndoa hizo, pia imebainika kwamba asilimia 99 ya ndoa hizo
hazidumu. Harieth Kulwa ni mmoja wa waathirika wa ndoa hizi ambaye ndoa yake
imevunjika."Nilidhai kuolewa ndio kutatatua matatizo yangu, kumbe
nilijiongezea matatizo. Mwanamume aliyenioa kwanza alikuwa mkubwa kwangu, pili
alikuwa mlevi…" Anabainisha Harieth.
Hata hivyo, wanaharakati wa haki za
binadamu wanaulalamikia mfumo mzima wa kusimamia sheria kwa kutowachukulia hatua
kali za kisheria watu wanaobainika kuwasababishia mimba watoto, wakidai kuwa ni
kutokana na vitendo vya rushwa vilivyogubika vyombo vya shERIA.
BBC SWAHILI
BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment